KIST YASHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA ICECCME

2025-10-16 11:33:45 category

VYUO vikuu vya Tanzania ikiwemo Zanzibar vimeshauriwa kufanya tafiti za pamoja za matumizi ya Kompyuta,mawasiliano na ubunifu ili kuongeza ubora wa elimu hapa nchini.

 

Akifungua mkutano wa kimataifa wa masuala ya Kompyuta,ubunifu na mawasiliano huko Mbweni uliozishirikisha nchi zaidi ya 58 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  Ndg, Khamis Abdalla Said alisema tafiti hizo zitakuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania kwenye masuala ya mawasiliano katika kukuza uchumi wa kidigitali kupitia viwanda.

 

Alisema Tanzania hivi sasa imejikita katika kuongeza ujenzi wa viwanda katika maeneo mbalimbali hivyo tafiti za pamoja zinazofanywa na vyuo vikuu kutoka Tanzania kwa kushirikiana na vyuo vya Ulaya zitakuwa na uwezo wa kuongeza utaalamu wa kutumia kompyuta na kuongeza ubunifu kwa wataalamu na watafiti hao.

 

Alisema kufanyika kwa mkutano huo hapa nchini kutatoa nafasi kwa mainjinia wa Tanzania kubadilishana uzoefu juu ya matumizi ya teknolojia ya kompyuta na kuongeza ubunifu wa mawasiliano.

 

“Hii ni fursa adhimu kwa Taasisi ya Karume (KIST), Chuo kikuu cha Zanzibar SUZA za kujua changamoto za mawasiliano na maendeleo ya sayansi kwenye kompyuta na vipi vyuo vikuu vinaendeshwa duniani”, alisema.

 

Alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa   kupitia mkutano huo vyuo vitapata maazimio ya dunia kuhusu maendeleo ya sayansi ya mitandao kupitia mawasiliano hasa uendeshaji wa vyuo vikuu.

 

Alisema Tanzania inaingia katika sera ya matumizi ya Tehama kwa kuzingatia dira ya maendeleo endelevu ya 2020-2050 ambayo inahimiza uchumi wa kidigitali hivyo kukutana kwa wataalamu hao hapa Zanzibar wataongeza utaalamu kwenye masuala ya kompyuta.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST), Dk. Mahmoud Abdulwahab Alawi alisema mkutano huo unalengo la kuangalia machapisho mbalimbali yaliyochapishwa kutoka vyuo vikuu vya kimataifa duniani katika kubadilishana uzoefu na vyuo vya Tanzania.

 

Alisema machapisho hayo yamewakutanisha wasomi wa vyuo vikuu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania pamoja na Zanzibar ambao pia watabadilishana uzoefu juu ya kufanya utafiti kwenye vyuo vikuu.

 

Alisema Zanzibar kuandaa mkutano kama huo ni kuonyesha mashirikiano yaliyopo kati ya vyuo vikuu vya Tanzania na dunia katika kuimarisha mawasiliano kwenye sekta ya elimu.