Mon, Jan 19, 2026
  Email: info@kist.ac.tz    
WAZIRI wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina matumaini makubwa ya vijana wanaohitimu na kuwa nguzo muhimu katika kuleta mageuzi ya kidigitali, ajira na maendeleo endelevu ya Taifa.
Waziri Soraga amesema hayo wakati akizungumza katika mahafali ya 11 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) yaliyofanyika Chukwani, Unguja.
Alisema Serikali inaamini kuwa maarifa na ujuzi walioupata wahitimu hao yatachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya Taifa iwapo yatatumika ipasavyo katika soko la ajira, ujasiriamali na kutatua changamoto za kijamii.
“Ni matumaini yetu kuwa kile mlichokijifunza kitailetea Taifa manufaa makubwa kwa kuitumia taaluma mliyoipata kwa vitendo,” alisema.
Aidha, aliipongeza KIST kwa kazi kubwa ya kuwaandaa vijana kitaaluma katika fani mbalimbali za sayansi, teknolojia na mafunzo ya amali na kuwa jitihada hizo zinaendana na dira ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidigitali unaoongozwa na maarifa na ubunifu.
Alifahamisha kuwa Wizara yake itaendeleza ushirikiano mzuri na taasisi za elimu katika kukuza sekta ya sayansi, teknolojia ya habari na ubunifu nchini.
Sambamba na hayo, aliwataka wahitimu hao kutoishia kwenye elimu waliyoipata chuoni, bali waendelee kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani.
“Msiridhike na elimu hii mliyoipata, mnatakiwa kuendelea kujiendeleza, kwani elimu haina mwisho,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Karume Dkt. Afua Khalfan Mohamed, aliiomba Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wake na taasisi hiyo ili kuwajengea uwezo wahitimu katika soko la ajira na kuwapa ujuzi unaoendana na ushindani wa dunia ya leo.
Dk. Afua alisema KIST ina dhamira ya dhati ya kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa, sambamba na kuwajenga kuwa wabunifu na wenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada zake za kuhakikisha KIST inachangia kikamilifu maendeleo ya nchi, ikiwemo hatua ya kuunda Wizara maalumu inayosimamia masuala ya Teknolojia ya Habari na Ubunifu.
Aliwataka wahitimu kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kutumia maarifa waliyojifunza, huku akiwahimiza kuwa mabalozi wazuri wa taasisi yao na Taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa Baraza la Taasisi litaendelea kusimamia na kuhakikisha KIST inaendelea kutoa elimu yenye ubora, inayozingatia maadili, ubunifu na mahitaji ya maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Naye, Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, Dk. Mahmoud Abdulwahab Alawi, alisema jumla ya wahitimu 1,039 wametunukiwa vyeti mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2024/2025.
Alifafanua kuwa kati ya wahitimu hao, wanawake ni 334 na wanaume 705, waliotunukiwa vyeti vya Shahada, Stashahada ya Juu, Stashahada na Astashahada katika fani tofauti.
“KIST kwa sasa inatoa fani 11 za Mafunzo ya Amali, programu 18 za Astashahada na programu nne za Shahada,” alisema.
Awali, akisoma risala ya wahitimu, Omar Juma Mohamed, alitoa shukrani za dhati kwa wakufunzi wao kwa kuwalea na kuwafundisha siyo tu taaluma, bali pia maadili ya kazi, uzalendo na uwajibikaji.
Alisema wahitimu wako tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa na kuchangia maendeleo chanya katika mazingira ya ushindani kwa kutumia ujuzi walioupata kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia wanafunzi mikopo na misaada ya kujikimu katika kuendelea na masomo bila vikwazo.