KIST YAFUNGUA TAWI PEMBA.

2025-09-19 10:02:38 category

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AMEFUNGUWA TAWI LA KIST PEMBA.

Kufunguliwa kwa Tawi la Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) Kisiwani Pemba kunatarajiwa kusogeza karibu huduma za masomo ya Sayansi na Teknolojia kwa wananchi na kutoa fursa kwa vijana kujiendeleza kielimu wakiwa Pemba badala ya kulazimika kufuata masomo nje ya kisiwa hicho.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema hayo alipofungua rasmi Tawi la KIST Pemba katika hafla iliyofanyika viwanja vya Mnazimmoja Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

 

Mhe. Hemed amesema Taasisi ya KIST imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza taaluma ya Sayansi na Teknolojia ndani na nje ya nchi, sambamba na kuandaa wataalamu wengi wa fani hizo nchini na Barani Afrika.

 

Aidha, uwepo wa Tawi la Pemba utasaidia kuitangaza Pemba kielimu, kuwavutia wanafunzi na watafiti, pamoja na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma mbalimbali.

 

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kupitia uboreshaji wa miundombinu, ubora wa elimu na maslahi ya walimu, hatua ambazo zimechangia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

 

Aidha, amesema Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar hadi kufikia shilingi bilioni 37.5 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua itakayowanufaisha zaidi ya wanafunzi 14,000, wakiwemo wanafunzi wapya na wale wanaoendelea, huku pia wanafunzi wa ngazi ya diploma wakitarajiwa kunufaika kwa mara ya kwanza.

 

Sambamba na hilo, Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar hadi kufikia shilingi bilioni 864 kwa mwaka 2025/2026 kwa lengo la kuendeleza mapinduzi ya kielimu ili kuendana na mabadiliko ya dunia na mahitaji ya soko la ajira.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amewatoa hofu wanafunzi na wakufunzi wa KIST Pemba akibainisha kuwa Tawi kubwa na la kisasa litajengwa kisiwani humo ili kuwezesha utoaji wa elimu kwa kiwango cha juu.

 

Waziri Lela pia amewataka wazazi na wananchi kutumia fursa ya Tawi hilo kwa kuwasajili vijana wao, akisisitiza kuwa elimu inayotolewa na KIST ni yenye ubora wa kimataifa.