KIST IMEPOKEA UGENI KUTOKA UBALOZI WA MAREKANI NCHINI TANZANIA.

2026-03-23 10:43:19 category

KIST IMEPOKEA UGENI KUTOKA UBALOZI WA MAREKANI NCHINI TANZANIA.

 

Uongozi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) umepokea ugeni maalum kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, uliowasili leo tarehe 23 Machi 2026 kwa lengo la kufanya ziara na kujionea maendeleo ya Taasisi hiyo, hususan katika nyanja ya kitaaluma.

 

Ugeni huo uliongozwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Andrew Lentz, akiwa ameambatana na ujumbe wake.

 

Katika ziara hiyo, walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi ikiwemo karakana za Taasisi ambazo wanafunzi wanapata ujuzi wa kitaaluma ambao utawasaidia kuajiriwa au kujiajiri .

 

Uongozi wa Taasisi ulieleza kuwa KIST imepiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha zaidi ya miaka sitini (60) tangu kuanzishwa kwake. Mafanikio hayo yanajumuisha kuongezeka kwa programu mbalimbali za masomo katika ngazi za Diploma na Degree, uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Taasisi hiyo katika fani mbalimbali.

 

Aidha, uongozi ulisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi endelevu za kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ubunifu, na kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaokidhi viwango vya kimataifa.

 

Ugeni huo ulieleza kufurahishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Taasisi hiyo, na kusisitiza kuwa utaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Ubalozi wa Marekani na Taasisi ya Karume, hususan katika maeneo ya elimu, ubunifu na maendeleo ya Teknolojia.

 

 

Ziara hiyo inaonesha kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa na kuthibitisha nafasi ya Taasisi ya Karume kama kituo muhimu cha kukuza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini.