WANAFUNZI WATANO KIST KWENDA NCHINI UTURUKI.

2026-03-20 12:09:04 category

WANAFUNZI WATANO KIST KWENDA NCHINI UTURUKI.

 

Uongozi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) leo tarehe 20, Machi, 2026, umefanya kikao maalum na Wanafunzi kutoka Idara ya Mawasiliano ya Anga, Elektroniki na Kompyuta, wanaotarajiwa kusafiri kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya mafunzo mafupi katika Chuo Kikuu cha Aksaray (AKSARAY UNIVERSITY).

 

Katika kikao hicho, Uongozi wa Taasisi uliwahimiza Wanafunzi hao kutumia vyema fursa hiyo adhimu ya kielimu kwa kuzingatia malengo yaliyowapeleka, kujikita katika masomo yao, na kuwa mabalozi wazuri wa Taasisi pamoja na Nchi kwa ujumla.

 

Aidha, Uongozi uliwasisitiza kujiepusha na mienendo isiyofaa ambayo inaweza kuathiri safari yao ya kitaaluma na kupelekea sifa mbaya kwa Taasisi ya Karume na Nchi kwa ujumla.

 

Kupitia safari hiyo, Taasisi ya Karume imesema, Wanafunzi hao watapata uzoefu wa kimataifa, kuimarisha ujuzi wao wa kitaaluma, na kujifunza teknolojia za kisasa zitakazowasaidia katika maendeleo yao ya baadaye.

 

Pia Safari hiyo ni ishara ya dhamira ya Taasisi ya Karume katika kuendeleza elimu bora yenye viwango vya kimataifa, na kuwaandaa Wanafunzi kuwa wataalamu wenye ushindani katika soko la ajira Duniani.

 

Taasisi ya Karume ina ushirikiano mzuri wa kitaaluma na Chuo Kikuu cha Aksaray, ambapo hufanyika programu za kubadilishana Wanafunzi na Wakufunzi kwa lengo la kukuza maarifa, Utafiti, na Ubunifu, Ambapo Ushirikiano huo unaendelea kufungua milango ya fursa kwa Wanafunzi na Wakufunzi kujifunza katika mazingira ya kimataifa na kubadilishana uzoefu wenye tija.

 

Jumla ya Wanafunzi watano (5) wanasafiri, wakiwemo Wanawake wawili (2) na Wanaume watatu (3) wanaosoma fani ya Electrical and Electronic Engineering pamoja na Telecommunication and Networking Engineering, kwa ngazi ya Degree mwaka wa tatu.