Fable robot presentation at Takwimu House

ALI SULEIMAN

Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar mhe, Simai Mohammed Said amesema serikali kwa kushirikia na sekta binafsi imekuwa ikiimarisha miundombinu ya Elimu ya Sayansi na teknolojia ili kuendana na kasi ya maendeleo katika karne hii

Akifungua warsha ya elimu ya kiroboti, katika ukumbi wa ofisi ya mtawimu mkuu wa serikali Mazizini mjini Unguja amesema lengo la kufanya hivyo ni kutokana na umuhimu wa ongezeko la matumizi ya teknolojia kwa maendeleo endelevu nchini.

Amesema kwa sasa mabadiliko ya sayansi na teknolojia yamekuwa yakiibua idadi ya watu wenye ujuzi wa masuala hayo pamoja na kukuza ajira hivyo kunahitaji zaidi kutengenezewa mazingira rafiki ili kwenda sambamba na ukuaji huo wa sayansi na teknolojia.

Mhe Simai amesema hivi sasa dunia ipo katika karne ya sayansi na teknolojia na Zanzibar nayo pia ni sehemu ya dunia, hivyo ni lazima iendane na kasi ya mabadiliko ya karne hii ambapo imewekwa mikakati muhimu na mataifa mbalimbali ulimwenguni kwa kujenga mashirikiano kati ya serikali na taasisi zisizokuwa za kiserikali katika kuimarisha miundombinu ya sayansi na teknolojia na kuwajengea uwezo wa kielimu watendaji wao ili waendane na kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.

Aidha mhe Simai amefahamisha kuwa Tanzania kwa kushirikiana na serikali zote mbili zimefanya jitihada kubwa za kujenga mashirikiano na sekta binafsi na asasi za kiraia kartika kuimarisha miundombinu ya sayansi na teknolojia na elimu ili nchi iendane na kasi ya maendeleo ya ishirini na moja.

Hata hivyo mhe Simai amesema Serikali Ya Mapinduzi Zanzibar imeimarisha njia za mawasiliano kwa kujenga mkonga wa taifa wa mawasiliano ambao umesambazwa nchi nzima, kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu katika fani ya teknolojia pamoja na kuimarisha mashirikiano mazuri kati ya serikali na sekta binafsi

Nae mkurugenzi Idara ya Teknolojia na Mawasiliano Wizara ya Elimu Na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw Omar Said Ali amesema lengo la warsha hiyo ni kuangalia kwa kiwango gani elimu hiyo ya kiroboti inaweza kuongeza ubunifu na ufahamu kwa masomo ya sayansi ikiwemo uhandisi na hesabati.

Warsha hiyo imefanyika kufuatia ziara ya mhe Simai nchini Botswana mwezi Agosti mwaka huu ambapo alikutana na kampuni ya Shape Robotics ya nchi hiyo na kuiomba kuja zanzibar kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa Elimu ili kukuza Elimu ya Tehama nchini.

Pia warsha hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Elimu Zanzibar kwa kushirikiana na kampuni ya Shape Robotics kutoka Botswana, imewashirikisha wadau kutoka taasisi mbali mbali za kielimu ambao walieleza uwezo wao katika masuala ya sayansi ambapo lengo kuweza kuanzisha mradi wa majaribio kwa Zanzibar na hatimae kueneza Afrika nzima

Related Posts you may like