Naibu Waziri awataka walimu kuwa na mashirikiano kazini

ALI SULEIMAN

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amewataka Walimu kuwa na mashirikiano kazini ili kuleta ufanisi wa kazi zao na kusaidia kutoa wataalam walio bora katika fani mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano na watendaji wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume (KIST), katika ukumbi wa Taasisi hiyo Mbweni Unguja, amesema ni vyema kuondosha ubinafsi baina yao ili kuleta maendeleo katika elimu nchini.

Amesema Walimu kufuata mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na kuwa wabunifu kwa kutumia mbinu mbadala katika ufundishaji, kutaweza kuwasaidia kuleta Mapinduzi katika masomo na kuwafanya Wanafunzi wao waweze kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira kutoka Serikalini.

Aidha amewataka Walimu hao kuzidisha bidii katika kazi yao pamoja na kuwa na subira kutokana na matatizo yaliopo katika Taasisi hiyo, huku akiwaahidi kuwa Wizara itaendelea kuyatatua matatizo hayo hatua kwa hatua.

Akizungumzia juu ya ombi kwa Taasisi hiyo juu ya kushiriki katika Maonesho ya Sababa Jijini Dar es salaam, Mhe. Simai amewahakikishia kuwa Wizara itajitahidi kufanya uwezekano ili Taasisi hyio mwakani iweze kushiriki katika maonesho hayo.

Nae Katibu Mkuu Dkt.Idrissa Muslim Hija akijibu baadhi ya Hoja za wafanyakazi hao juu ya suala la bima ya Afya, amesema hivi Sasa sera ya Serikali ni kutoa huduma ya matibabu bure,hivyo si ruhusa kwa Taasisi yeyote ya Serikali kuwalipia wafanyakazi wake Bima ya Afya kutoka katika pesa za Serikali, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na tamko la sera hiyo.

Amefahamisha kuwa mfanyakazi yeyote anaruhusiwa kukata bima kwa malipo yake mwenyewe, au endapo Taasisi itakuwa na mfumo wa kukusanya pesa wao wenyewe kwa utaratibu wao waliokubalina hakutakua na tatizo kufanya hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia,( KIST) bw Mustafa Ali Garu amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliopatikana katika kuzalisha wataalamu nchini, lakini bado miundombinu haitoshelezi ikiwemo madarasa na ofisi, udogo wa dakhalia pamoja na uhaba wa Walimu wenye kiwango cha kufundisha Shahada ya kwanza mbayo inatarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.

Nao baadhi ya Wafanyakazi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume wameiomba Wizara ya Elimu Zanzibar kutenga fungu maalum kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufundishia, kwani baadhi ya vifaa hawana kabisa na vilivyopo vimeshachakaa, hivyo ni muhimu kupata vifaa vya ziada ili viweze kuwasaidia Wanafunzi wao kusoma kwa nadharia na vitendo kwa lengo la kupata wataalamu bora nchini kwa maendeleo ya Taifa.

Related Posts you may like